RIADHA: Mbio za Diamond League kuanza kampeni zake jijini Rabat, Morocco Mei
2020-11-27 16:47:00| cri

Waratibu wa mbio za Diamond League wamefichua kalenda ya mashindano hayo katika msimu ujao wa 2021. Kwa mujibu wa ratiba hiyo, kampeni hizo zitajumuisha duru 14 za riadha zitakazoanzia jijini Rabat, Morocco mnamo Mei na kumalizikia Zurich, Uswisi mnamo Septemba.

Jiji la Doha nchini Qatar litakuwa mwenyeji wa duru ya Mei 28 kabla ya Roma nchini Italia kuandaa duru ya Juni 4, kisha Oslo nchini Norway (Juni 11). Duru za Stockholm, Monaco na London zimeratibiwa kufanyika katika kipindi cha majuma mawili ya mwanzo wa Julai. Baada ya likizo ya mwezi mmoja itakayopisha Olimpiki za Tokyo nchini Japan, mashindano ya Diamond League yatarejea kwa duru ya Shanghai mnamo Agosti 14 kabla ya Eugene (Agosti 21) kisha China iandae duru nyingine kwa mara ya pili mnamo Agosti 22. Duru za mwisho zitafanyika barani Ulaya katika majiji ya Lausanne, Paris na Brussels kabla ya fainali ya msimu kufanyika Zurich kati ya Septemba 8-9. Kwa mujibu wa waandalizi wa mbio za Diamond League, ratiba iliyotolewa kwa minajili ya kampeni za msimu wa 2021 si ya mwisho na huenda ikabadilika kutegemea hali ya maambukizi ya virusi vya corona duniani.