Maonesho ya 17 ya China-ASEAN na Mkutano wa kilele wa China na ASEAN kuhusu biashara na uwekezaji wafunguliwa
2020-11-27 16:48:14| CRI

Maonesho ya 17 ya China-ASEAN na Mkutano wa kilele wa China na ASEAN kuhusu biashara na uwekezaji wafunguliwa

Rais Xi Jinping wa China leo amehutubia ufunguzi wa maonesho ya 17 ya China na ASEAN na Mkutano wa kilele wa China na ASEAN kuhusu biashara na uwekezaji. Rais Xi amesisitiza kuwa China inapenda kushirikiana na Jumuiya ya ASEAN kusukuma mbele ushirikiano kwenye nyanja mbalimbali, kudumisha mwelekeo mzuri wa maendeleo na ustawi kwenye kanda hiyo, na kujenga jumuiya yenye mustakbali wa pamoja kati ya pande hizo mbili. 

Kwenye hotuba yake, Rais Xi Jinping wa China amepongeza maendeleo yaliyopatikana katika miaka ya hivi karibuni kwenye uhusiano kati ya China na ASEAN. Anasema,

“Mwaka 2013, nilitoa pendekezo la kushirikana na nchi wanachama wa ASEAN kwenye ujenzi wa njia ya hariri ya baharini ya karne 21, na kujenga kwa pamoja jumuiya yenye ukaribu zaidi ya hatma ya pamoja kati ya China na ASEAN. Katika miaka saba iliyopita, uhusiano kati ya China na ASEAN umekuwa mfano wenye mafanikio zaidi na wenye uhai zaidi kwenye ushirikiano wa kanda ya Asia na Pasifiki, na pia umekuwa kielelezo wazi cha kusukuma mbele ujenzi wa jumuiya ya binadamu yenye hatma ya pamoja.”

Rais Xi amesema, China na ASEAN zimekuwa zikijaliana na kusaidiana wakati wa kukabiliana kwa pamoja na janga la virusi vya Corona. Dunia ya leo inashuhudia mabadiliko makubwa ambayo hayajawahi kutokea katika miaka 100 iliyopita, na hatma ya watu wa nchi mbalimbali duniani imeunganishwa kwa karibu zaidi. Amesema China inatoa kipaumbele kwa jumuiya ya ASEAN kwenye diplomasia yake ya kikanda na kuichukulia kuwa eneo muhimu la ushirikiano kwenye ujenzi wa “Ukanda Mmoja, Njia Moja”, China inapenda kushirikana na ASEAN katika kuendeleza ushirikiano kwenye nyanja mbalimbali, kulinda mwelekeo mzuri wa maendeleo kwenye kanda hiyo, na kujenga jumuiya yenye ukaribu zaidi ya hatma ya pamoja kati ya pande hizo mbili.

Kwenye hotuba yake, Rais Xi ametoa mapendekezo manne ya kutimiza lengo hilo. Kwanza ni kuinua kiwango cha kuaminiana kimkakati na kuunganisha kwa kina mikakati ya maendeleo; Pili ni kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi na kibiashara, na kuharakisha ufufukaji wa uchumi wa kikanda kwa pande zote; Tatu ni kuhimiza uvumbuzi wa sayansi na teknolojia, na kuimarisha ushirikiano katika uchumi wa kidijitali; Nne ni kupanua ushirikiano kwenye mapambano dhidi ya virusi vya Corona, na kuimarisha ujenzi wa uwezo wa afya ya umma.

Rais Xi amesisitiza kuwa mwaka kesho China itazindua safari mpya ya kuelekea kujijenga kuwa nchi ya kisasa ya Usoshalisti. China itaendelea kufungua mlango zaidi kwa nje, na hakika China na ASEAN zitakuwa na mustakbali mkubwa zaidi wa ushirikiano.