Mchango wa kipekee wa China katika mapambano dhidi ya janga la corona duniani utakumbukwa daima
2020-12-29 13:34:18| cri

Na Eric Biegon

 Iwapo kuna wakati ambapo mataifa yametakiwa kusimama kwa pamoja na kuepuka athari mbaya zaidi kutokea duniani, ni sasa. Mara nyingi tunasema tunaishi katika jumuiya ya kimataifa, au ulimwengu umekuwa kijiji. Ukweli ni kwamba, mgogoro wa sasa wa kiafya ulimwenguni unaonekana kufanya maneno haya kuwa halisi zaidi.

Virusi vya Corona vililipuka mwanzoni mwa mwaka huu wa 2020 na kuenea haraka kwenye pembe zote za dunia kama moto wa msitu unaosambaa kwa kasi. Tangu wakati huo, janga hilo limemsukuma na kumfikisha binadamu ukingoni, na kuwa pigo kubwa kwa mwanadamu kwa kiwango ambacho hakijashuhudiwa katika kumbukumbu za hivi karibuni.

Hatari kubwa ya janga la virusi vya Corona ni kwamba, halina upendeleo wala halijali hali ya kijamii na kiuchumi, na wala halijali jinsia, rangi, au dini. Nchi tajiri na maskini zote zimeathirika vibaya kutokana na virusi hivyo ambavyo havitambui mipaka.

Kama mataifa yaliyo na uwezo mkubwa kiuchumi yanashindwa kudhibiti maambukizi ya virusi hivi, itakuwaje kwa mataifa maskini zaidi duniani, ambayo mengi yako barani Afrika? Lakini shukrani kwa China, kwani msaada uliwasili, na uliwasili kwa wakati ufaao. Baada ya kufanikiwa kudhibiti maambukizi ya virusi, China mara moja ilianza kupambana bega kwa bega na nchi nyingine katika vita dhidi ya janga hilo. 

Toleo maalum lililochapishwa na serikali nchini humo mara tu baada ya maradhi hayo kutambulika liligonga vichwa vya habari. Ndani yake, China ilishiriki uzoefu wake katika mapambano dhidi ya virusi hivyo huku ikitangaza utayari wake kushirikiana na ulimwengu, hasa Afrika katika juhudi hizo.

Itakumbukwa kuwa, Rais wa China Xi Jinping alikuwa kiongozi wa kwanza wa nchi kubwa kiuchumi duniani kutoa wito wa ushirikiano wa kimataifa katika kupambana na janga la virusi vya Corona. Akizungumzia usumbufu uliosababishwa na janga hilo, rais Xi alitoa wito wa juhudi za pamoja huku akielezea wasiwasi wake kwamba, maambukizi hayo yanaendelea kuongezeka na kusababisha maafa zaidi.

Alisema mgogoro huu wa afya umedhihirisha ukweli kwamba jamii ya binadamu ni jamii yenye mustakabali wa pamoja, na ni kupitia kuungana mkono tu ndipo nchi zote zinaweza kujiondoa kutoka kwa janga kama hili.

Hii haikuwa ahadi tupu, kwani Rais Xi alitangaza kuchangia dola za kimarekani milioni 50 kwa Shirika la Afya Duniani (WHO) ili kuongeza juhudi zake za kupambana na kuenea kwa virusi hivyo. Muda mchache baadaye, serikali yake ikatoa vifaa tiba vya dharura kwa zaidi ya nchi 150 na mashirika ya kimataifa.

Mchango mwingine ambao hauwezi kusahaulika ni ule uliotolewa na mfanyabiashara maarufu kutoka China Jack Ma, ambaye alitoa vifaa mbalimbali vya kukabiliana na virusi hivyo kwa kila nchi barani Afrika, vikijumuisha barakoa, vitakasa mikono pamoja na vifaa vingine vya kinga binafsi.

Ndani ya miezi mitano, China ilisafirisha zaidi ya barakoa bilioni 152, mavazi ya kujikinga bilioni 1.4, miwani milioni 230, mashine za kupumua 209,000, vifaa vya upimaji vilivyo na uwezo wa kutumika kwa watu milioni 470 na vipimajoto milioni 81.

Wakati wa mkutano wa jukwaa la Baraza la Afya Duniani uliofanyika mwezi Mei, Rais Xi alitangaza hatua mpya zitakazochukuliwa na taifa lake ili kusaidia juhudi hizo. Alisema China itatoa dola bilioni 2 za Marekani kusaidia katika vita dhidi ya virusi vya Corona, zitakazoelekezwa kwa nchi zilizoathirika zaidi kiuchumi, hasa nchi zinazoendelea. Pia aliahidi kuwasaidia watu wengi zaidi katika bara la Afrika, kupitia utaratibu wa ushirikiano ambapo hospitali za China zilipaswa kuungana na zile za Afrika.

Kilichofuatia ni mikutano mingi kati ya wataalamu wa afya wa China na wenzao wa Afrika, kubadilishana uzoefu katika kukinga virusi hivi, jambo lililosaidia sana kwani nchi hizo zilikuwa zinapambana na adui ambaye hakuna aliyejua chochote kumhusu.

China haikuishia kwenye kutoa misaada pekee, bali pia iliwasilisha masuala ya bara la Afrika kwenye jukwaa la kimataifa. Rais Xi alizishawishi nchi wanachama wa Kundi la Nchi 20 (G20) kutekeleza mpango wa kusitisha ulipaji wa madeni kwa nchi ambazo zimeathirika zaidi kiuchumi kutokana na janga hilo. Hii ilitoa nafuu kwa mataifa ambayo muda wa kulipa mikopo yao ulikuwa umewadia.

Baada ya muda, ilidhihirika kuwa janga hilo halitamalizika haraka kama ilivyotarajiwa awali, na macho yote yakaanza kuangazia upatikanaji wa chanjo. Ni jambo la kutia moyo kwamba China imeahidi kuwa mara tu chanjo yake ya virusi vya Corona itakapoanza kutumika, nchi za Afrika zitakuwa miongoni mwa mataifa ya kwanza kunufaika.

Bila shaka, hali sio mbaya sana barani Afrika ikilinganishwa hali ilivyo katika mataifa mengine, hata hivyo, hatua zilizochukuliwa na China zimesaidia kuokoa idadi kubwa ya maisha ya watu, na mchango huu kwa Afrika unatoa matumaini zaidi juu ya siku za usoni.

Katika wakati kama huu, ni wazi kwamba utengano unafanya dunia kuwa dhaifu, ilhali umoja unahakikisha uthabiti wa binadamu. Kile ambacho China imeonyesha ni kwamba, kupitia ushirikiano ni rahisi kushinda matatizo ya kila aina.

Wakati virusi hivi vitakaposhindwa, China itakumbukwa kwa kutoa msaada wake hasa kwa wale wasiojiweza.