Makamu wa Rais Tz Samia Suluhu aagiza kila halmashauri kuwa na kiwanda cha kuchakata mazao ya nyuki na misitu
2021-02-25 19:46:58| cri

Makamu wa Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, ameagiza kila halmashauri nchini humo kuwa na kiwanda cha kuchakata mazao ya nyuki na kuboresha viwanda vya uzalishaji wa mazao ya mbao.

Katika hotuba yake iliyosomwa na Waziri wa Maliasili na Utalii Dk. Damas Ndumbaro, wakati wa uzinduzi wa kongamano la kimataifa la sayansi juu ya mnyororo wa thamani wa mazao ya misitu na nyuki kwa ajili ya maisha endelevu na uchumi wa viwanda,Samia alisema viwanda vya kuchakata mazao ya nyuki kwa sasa vipo 21, lakini wizara imeongeza viwanda vitatu kwa hiyo kutakuwa na viwanda 26 ambavyo bado havitoshi, na kuongeza kuwa katika hali ya kawaida viwanda vidogo vinatakiwa vile 200.

Alisema Tanzania ina jumla ya halmashauri 186,kwa hiyo kila halmashauri inatakiwa kuwa na kiwanda kimoja ambacho nacho hakitoshi lakini itakuwa angalau.

Alisema kuwa uwezo wa nchi wa kuzalisha asali ni tani 134,000, lakini kwa sasa nchi inazalisha tani 34,000 tu,aliongeza kuwa ipo haja ya kuongeza kiwango hico.

Aidha Samia aliagiza kila halmashauri nchini humo kuhakikisha inapanda miti milioni 1.5 kila mwaka.