Sekta ya Utalii eneo la Pwani Kenya yaendelea kudorora kufuatia janga la Corona
2021-02-25 19:47:24| cri

 

Wawekezaji katika sekta ya utalii nchini Kenya ,hasa eneo la Pwani , wanaendelea kukadiria hasara kufuatia janga la korona ambalo limesababisha kuzorota kwa uchumi.

Hoteli nyingi za Pwani sasa hivi zina kiwango kidogo cha wageni.Wenye hoteli wanaandikisha asilimia 20 ya wageni huku msimu wa chini wa wageni ukianza baada ya mwaka mgumu wa utalii wa 2020 kufuatia janga la korona.

Hoteli nyingi ambazo zilikuwa zikitegemea watalii wa ndani baada ya wale wa kimataifa kusitisha usafiri kutokana na janga la korona zimebakia bila wageni.

Mwenyekiti wa chama cha Wawekezaji wa Utalii nchini Kenya Bw Mohamed Hersi amesema wageni wa humu nchini ndio wamekuwa wakipiga jeki sekta hiyo,ingawa kwa kiasi kidogo.

Hersi amesema kutojulikana kwa hatima ya janga la korona kunazidi kutishia utalii.

Aidha aliongeza kuwa kutokuwa na uhakika kumewalazimisha wamiliki wa hoteli kuanza kubuni mbinu mbalimbali za kukuza soko la ndani na vivutio vingine.

Wakati huo huo Hersi alisema wawekezaji hao wamelazimika kupunguza ada za hoteli.