Bodi ya Utalii Tanzania kuwaelimisha wanawake kuchangamkia fursa katika sekta ya Utalii
2021-02-25 19:47:47| cri

Bodi ya Utalii Tanzania(TTB), inatarajia kuwakutanisha wanawake kutoka katika mikoa mitatu ya Dar es Salaam, Arusha na Mwanza  kwa ajili ya kuwaelimisha namna ya kuchangamkia fursa mbalimbali zilizopo katika sekta ya utalii nchini humo.

Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi hiyo, Devotha Mdachi, alisema tukio hilo litafanyika Machi 8, mwaka huu katika maadhimisho ya siku ya mwanamke duniani, na kwamba lengo ni kuthamini mchango wao katika kukuza utalii.

Alisema ipo haja kwa wanawake kuhakikisha wanachangamkia fursa mbalimbali zilizopo katika sekta hiyo ikiwamo kumiliki makampuni makubwa yanayojihusisha na shughuli hizo za utalii.

Aidha alisema wanawake hawafai kuishia tu katika kufanya shughuli ndogo, wanafaa pia wafanye shughuli kubwa kama kumiliki makampuni yao wasiseme ni kazi zinazotakiwa kufanywa na wanaume peke yao.

Alisema katika madhimisho hayo, kutakuwa na kutembelea vivutio mbalimbali vya utalii na kufanya shughuli mbalimbali za kijamii.