Rais wa Zimbabwe aishukuru China kwa msaada wa pili wa chanjo ya COVID-19
2021-02-26 09:16:57| CRI

Rais Emerson Mnangagwa wa Zimbabwe ameishukuru China kwa kuipatia shehena ya pili ya msaada wa chanjo ya COVID-19.

Akiongea jana mjini Harare Rais Mnangagwa amesema amearifiwa kuwa Zimbabwe imepokea dozi laki mbili za chanjo kutoka kwa Rais Xi Jinping, serikali ya China na watu wa China, na kufanya jumla ya msaada huo kufikia dozi laki 4.

Amesema mbali na chanjo hiyo, Kampuni ya Sinopharm ya China imesema itatenga dozi nyingine milioni 1.8 zitakazonunuliwa na Zimbabwe, na kati ya dozi hizo, dozi laki 6 zinatarajiwa kufika Zimbabwe mwanzoni mwa mwezi Machi.

Serikali ya Zimbabwe ilianza mpango wa kutoa chanjo Alhamisi iliyopita, siku tatu baada ya shehena ya kwanza ya dozi laki mbili kufika kutoka China. Makamu wa Rais Bw. Constantino Chiwenga alikuwa wa kwanza kupata chanjo hiyo, pamoja na wafanyakazi wengine walio mstari wa mbele.