Wataalamu wa WHO watahadharisha kuhusu hatari za afya baada ya COVID-19
2021-02-26 09:17:54| CRI

Mkurugenzi wa kanda ya Ulaya wa Shirika la afya Duniani Bw. Han Kluge, amesema wakati maambukizi ya COVID -19 barani Ulaya yanapungua, kuna hatari ya kiafya inayotokana na kuwepo kwa maambukizi hayo kwa muda mrefu.

Amesema madhara ya maambukizi ya COVID-19 yanaendelea kuwepo kwa muda mrefu kwenye mambo ya kijamii, kiuchumi, afya na hata kwenye ajira, na kuwa suala hilo kwa sasa ni kipaumbele kwa WHO.

Bw. Kluge amesema hadi sasa watu milioni 38 wameambukizwa COVID-19 tangu ugonjwa huo uanze, na mmoja kati ya watu 10 anakuwa na hali mbaya ya afya kwa wiki 12, na hata muda mrefu zaidi. Na baada ya hapo kunakuwa na watu waliopona, lakini maisha yao yanakuwa yameathiriwa.

Amesema hivi karibuni WHO itaitisha mkutano wa maofisa wakuu wa afya wa nchi zote 53 kwenye eneo la Ulaya ili kuweka mkakati wa kikanda kukabiliana na jambo hilo.