Marais wa China na Ufaransa wafanya mazungumzo kwa njia ya simu
2021-02-26 09:44:46| CRI

Rais Xi Jinping wa China jana usiku alifanya mazungumzo na rais Emmanuel Macron wa Ufaransa kwa njia ya simu, ambapo walitumiana salamu za mwaka mpya, na kutoa salamu kwa watu wa nchi hizo mbili.

Rais Xi Jinping amesema mazungumzo waliyofanya mara 5 kati yao katika mwaka 2020 yalihimiza maendeleo ya uhusiano kati ya China na Ufaransa, na makubaliano yaliyofikiwa nao yalitekelezwa vizuri. Katika mwaka huu mpya, pande hizo mbili zinapaswa kuendelea na juhudi za kuhimiza maendeleo zaidi kwenye uhusiano kati ya nchi zao.

Amesema China inapenda kujadiliana na Ufaransa kuhusu kuanzisha ushirikiano wa pande tatu kwenye sehemu ya mashariki na kati ya Ulaya. Nchi hizo mbili pia zinapaswa kuhimiza jumuiya ya kimataifa kushikilia haki na usawa, kuendeleza majadiliano na ushirikiano, kuwa wazi na shirikishi, kutoa mchango kwenye mapambano dhidi ya janga la COVID-19 na kuhimiza amani na maendeleo ya dunia.

Kwa upande wake Rais Macron amesema Ufaransa inapenda kuongeza mawasiliano na China katika mambo ya kimataifa, na inatarajia kushirikiana na China kuhimiza jumuiya ya kimataifa kuzipunguzia madeni nchi za Afrika na kutimiza ongezeko la uchumi barani Afrika.