Sudan Kusini kutoa chanjo ya polio kwa watoto milioni 2.8
2021-02-26 09:17:27| CRI

Sudan Kusini kwa kushirikiana na Shirika la kuhudumia watoto la Umoja wa Mataifa UNICEF na Shirika la Afya Duniani WHO jana walianza kutoa chanjo ya polio kwa watoto milioni 2.8 nchini humo.

Mkurugenzi mkuu wa afya ya msingi wa wizara ya afya ya Sudan Kusini Bw. Atem Nathan, amesema mlipuko wa Polio ulitangazwa Septemba 18 mwaka 2020 na sasa umeenea kwenye kaunti 17 za nchi hiyo. Majimbo ya Warrap na Bahr El Ghazal Magharibi ndio yameathiriwa zaidi.

Mwakilishi wa WHO nchini Sudan Kusini Bw Olushayo Olu amesema ili kuzuia ugonjwa huo, wadau wameimarisha ufuatiliaji, na kuweka mkazo kwa jamii na vituo vya afya kufuatilia watoto ambao wamepooza miguu kwa ghafla.

Amesema kampeni ya sasa inalenga kutoa fursa kwa watoto walio kwenye hatari kupata uingiliaji wa haraka unaoweza kuepusha vifo na ulemavu kutokana na ugonjwa huo.