Umoja wa Afrika na vikosi vya Somalia wazindua kituo cha operesheni ya pamoja kupambana na kundi la al-Shabab
2021-09-24 09:04:10| CRI

Ujumbe wa Umoja wa Afrika nchini Somalia (AMISOM) na Jeshi la taifa la Somalia (SNA) wamezindua kituo cha operesheni cha pamoja huko Mogadishu ili kuimarisha juhudi zinazoendelea za kuleta utulivu nchini Somalia.

AMISOM imesema kwenye taarifa iliyotolewa jana kuwa kituo hicho cha pamoja, kitaimarisha upangaji wa pamoja na uratibu wa operesheni za kijeshi dhidi ya kundi la al-Shabab.

Mkuu wa vikosi vya jeshi la Somalia Bw. Odowaa Yusuf Rageh, amesisitiza ushiriki wa jeshi la Somalia, na umuhimu wa ushirikiano kati ya jeshi hilo na AMISOM katika kuendesha kituo hicho.

Naibu kamanda wa kikosi cha AMISOM Bw. William Kitsao Shume, anayesimamia shughuli na mipango, amesema kuzinduliwa kwa kituo hicho ni hatua muhimu katika kufikia lengo la pamoja la kuwa na vituo kama hivyo kote nchini Somalia.